Friday 5 November 2010

Marehemu Elvis Musiba

Marehemu Elvis Musiba
Wiki hii imekuwa ya misiba mikubwa kwa bendi, rafiki yetu Super Coach katutoka akifuatiwa na Patron wa Bendi Elvis Musiba. Uhusiano wa bendi na Marehemu Musiba ulianza miaka ya sabini wakati bendi bado inaitwa The Revolutions na ikipiga katika ukumbi wa Simba Grill, Kilimanjaro Hotel. Musiba mwanzoni alikuwa mpenzi tu wa muziki lakini akawa na ukaribu na wanamuziki kiasi cha kuanza kuwapa ushauri wa biashara ya muziki. Ukaribu uliendelea kiasi cha kuwa alianza kusafiri katika mikutano mbalimbali ya kibiashara na mmoja wa wanamuziki Waziri Ally, akiwa kama afisa wake ili ajifunze taratibu mbalimbali za biashara. Mwaka 1989 aliisafirisha bendi nzima ikiwa na wanamuziki 9 kwenda Uingereza kwa gharama zake,wanamuziki Mohamed Mrisho, Waziri Ally, Keppy Kiombile, Juma Omary, Mabrouk Khamis, Marehemu Chuky, Dullah, na dancers Marehemu Chilleshi Ally na Bahati waliishi London kwa gharama za Marehemu Musiba. Katika wakati huo aliitambulisha kwa producer mmoja ambaye aliwezesha bendi kurekodi album ya Katakata yenye ule wimbo maarufu wa Njenje. Bahati mbaya producer alipotea na fedha zilizopatikana na hajaonekana mpaka leo, lakini Musiba aligharamia bendi kuweza kununua vyombo , na kwa ushauri wake bendi ambayo kwa wakati huu ikawa imeshabadili jina na kujiita Kilimanjaro Band ilijiweka katika mfumo wa kibiashara zaidi na kuanzisha Kilimanjaro Band Company LTD, ambayo ndio imekuwa sababu kubwa ya bendi kuwa na wanamuziki wenye mshikamano  mpaka leo. Na kwa ushauri wa marehemu, Kilimanjaro Band pia ndio bendi pekee ambayo ni mwanachama wa Chamber of Commerce jambo ambalo limewezesha muziki kutambulika kama biashara muhimu kama nyingine.
 Marehemu Musiba alikuwa mwalimu kila ukikutana nae, pia alikuwa msanii wa kweli vitabu alivyotunga vyenye yule mbabe Willy Gamba katika Kikosi Cha Risasi na Nitakufa Nae na vingine vingi vinadhihirisha hilo. Pia Mzee Musiba ndie aligharamia kuanzishwa na kuweko kwa ile bendi iliyofurahisha wakati wake, bendi ya Tanza Muzika.
Baadhi ya wanamuziki wa Kilimanjaro Band wakiwa katika ratiba ya kuaga mwili wa Patron Musiba



Foleni ya kwenda kuaga mwili wa Musiba

Mungu amlaze pema peponi Elvis Musiba

No comments:

Post a Comment

ON STAGE

ON STAGE
ON STAGE

TUNAANZA MWAKA NA NGUVU MPYA